Tarehe 22 Desemba, 2014, Serikali ya Jamhuri ya Kenya ilitoa amri ya
kuzuia magari ya kitalii yenye usajili wa Tanzania kwenda kuchukua na
kushusha watalii wanaotumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo
Kenyatta wakiwa njiani kuja kutembelea vivutio vya utalii katika Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania.
Baada ya uamuzi huu wa Serikali ya
Kenya, Waziri wa Maliasii na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu alifanya
majadiliano na Waziri wa masuala ya utalii wa Serikali ya Kenya siku ya
tarehe 16, Januari, 2015 ili kutafuta ufumbuzi wa kadhia hii. Matokeo ya
mkutano wa Mawaziri hawa yalikuwa ni kusitishwa kwa muda katazo
lililotolewa na Serikali ya Kenya kwa makubaliano kuwa yafanyike
mazungumzo baina ya pande hizi mbili ndani ya kipindi cha wiki tatu
kuanzia tarehe 16 Januari, 2015 ili kurekebisha Mkataba wa Ushirikiano
katika sekta ya utalii wa mwaka 1985 kati ya nchi zetu mbili.
Kufuatia makubaliano hayo Wizara ya Maliasili na Utalii iliiomba Wizara
ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iandae kikao hicho cha pamoja
katika muda uliopangwa. Kwa kuzingatia historia na uzito wa suala
lenyewe, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iliona umuhimu wa
kuhusisha Wizara zingine husika za Uchukuzi, Mambo ya Nje, Viwanda na
Biashara, Fedha, Ulinzi, Mambo ya Ndani, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira na Viongozi wa Sekta Binafsi ili kupata
msimamo wa nchi wa pamoja kabla ya mkutano na Kenya.
Hivyo, vikao
vya wataalam vimefanyika Dar es Salaam na Arusha hadi wiki ya kwanza ya
mwezi huu wa pili kwa maandalizi ya kikao cha mwisho cha Mawaziri
upande wa Tanzania kabla ya kukutana na wenzetu wa Kenya. Pamoja na
kushauriana na Waziri mhusika wa Kenya (Masuala ya Afrika Mashariki,
Biashara na Utalii, Bi. Phyllis Kandie) kusogeza mbele tarehe ya mkutano
wa pamoja ili kuruhusu muda wa kutosha kwa majadiliano ya ndani na
wadau, Bi. Kandie alimwandikia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki, Dkt. Richard Sezibera na kumnakili Waziri Nyalandu, kurejesha
amri yake ya awali ambayo alisema inaendana na Sheria ya utalii na
kanuni za uchukuzi za Kenya.
Serikali ya Tanzania kimsingi
imesikitishwa na uamuzi huo wa Serikali ya Kenya kwani haujengi wala
hauendani na dhamira njema ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya kuenzi njia ya mazungumzo, maelewano na maridhiano katika
kufikia maamuzi. Suala la kurekebisha mkataba ulioingiwa na nchi hizi
mbili kwa hiari miaka 30 iliyopita, si jepesi la kujadiliwa na Mawaziri
wawili tu na kuwekeana ukomo wa muda katika kulipitia. Serikali ya
Tanzania itaendelea na mchakato iliouanzisha wa kuhusisha wadau wote na
kufikia uamuzi ambao itauwasilisha kwa Serikali ya Kenya kupitia vikao
rasmi vya Jumuiya.
Pamoja na kwamba amri hii ya Serikali ya Kenya
inaenda nje ya mkataba wa 1985 kwa kuvihusisha hata viwanja vya ndege
kuwa sehemu ya vivutio vya utalii, Serikali ya Tanzania itaheshimu na
kuzingatia amri hiyo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi
zetu huku tukitafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa
itakayotokea kwa watalii na wasafiri wetu wanaopitia uwanja huo wa Jomo
Kenyatta. Aidha Tanzania itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na
wageni wote wenye nia ya kutembelea vivutio vya kitalii vya Tanzania
kutumia viwanja vingine vya ndege ili kuepuka kadhia na gharama zisizo
za lazima.
Kwa upande wa Tanzania, viwanja vya ndege hasa vile
vya Kimataifa vitaendelea kuwa sehemu ya malango ya kuingilia na kutokea
kwenda kokote iwe ndani ya Jumuiya au nje ya Jumuiya na
havitavichukuliwa kama vivutio vya utalii. Tanzania haitazuia magari ya
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi nyingine yoyote
kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii
wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi zao.
Mkataba wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo
wa ushirikiano katika Sekta ya Utalii kati ya nchi zetu mbili. Aidha,
makubaliano hayo yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili ya kubadilishana
watalii huku ikizingatiwa kuondoa bugudha kwa watalii. Maeneo hayo ni
pamoja na miji ya mipakani pamoja na miji rasmi iliyopendekezwa na
kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi ambako kiwanja cha ndege
cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.
Mwisho, Tanzania itaendelea
kuenzi undugu na urafiki uliojengeka kwa zaidi ya miaka 50 tokea uhuru
kati ya nchi zetu mbili na suala dogo kama hili halitaweza kuteteresha
uhusiano wetu mzuri.
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
10 FEBRUARI, 2015.
10 FEBRUARI, 2015.
No comments:
Post a Comment