Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Profesa Benno Ndulu amesema hivi sasa sekta ya Utalii ndiyo inayoongoza
kwa kuliingizia taifa mapato ya kigeni baada ya kuipita sekta ya dhahabu
iliyoshuka kutokana na kuporomoka kwa bei kwenye soko la dunia.
Akizungumza
leo kwenye mkutano uliojadili mabadiliko ya kiuchumi Tanzania, Profesa
Ndulu amesema sekta ya utalii inaliingizia taifa dola 2bilioni, dhahabu
(dola 1.7bilioni), bidhaa za viwandani (dola 1.3bilioni) na huduma za
usafirishaji mizigo ni dola 800milioni.
Sekta ya utalii
inaingiza Dola za Marekani 2 bilioni kwa mwaka ikifuatiwa na dhahabu
inayoipatia nchi Dola za Marekani 1.7 bilioni, bidhaa za viwanda
vinazouzwa katika nchi mbalimbali barani Afrika inaingiza Dola za
Marekani 1.3bilioni ikifuatiwa na usafirishaji wa huduma za mizigo
katika nchi jirani ambapo zinaingiza Dola za Marekani 800milioni.
Profesa
Ndulu amesema ongezeko la mapato kwenye viwanda ni sawa na fedha zote
za kigeni zinazotokana na mazao sita makubwa ya kilimo nchini kwa
pamoja.
“Mfumo wa kuingiza mapato ya fedha za kigeni
nchini umebadilika sana, mimi na imani kuwa nafasi yetu kijiografia
inatupa fursa kubwa sana ya kuhudumia wengine walioko mbali na bahari,”
alisema Profesa Ndulu.
Akizungumzia kuhusu nafasi ya
kilimo, Profesa Ndulu almeema iwapo viwanda vingi vitajengwa karibu na
wakulima, mfumo wa uchumi katika maeneo hayo utaimarika kuliko ilivyo
sasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahimu Lipumba, alisema jambo muhimu linalotakiwa kujadiliwa ni namna
gani pato la viwanda litaongezwa zaidi kwa kuwa hivi sasa kuna
changamoto ya ukosefu wa umeme wa kutosha.
“Kwa muda
mrefu umeme umekuwa mdogo na ufisadi umeathiri sana sekta ya umeme kiasi
kwamba Tanesco inashindwa kuzalisha umeme wa kutosha kwa bei nafuu,”
amesema Profesa Lipumba.
Pia, amesema uwepo wa bandari
inayotumiwa na nchi jirani haujafanikiwa kuliingizia taifa mapato ya
kutosha kutokana na udhaifu ya kiuongozi.
“Uongozi wa
bandari unabadilika kila wakati, kila waziri akija anatafuta mtu wake
ambaye atamsaidia katika ulaji kwa hiyo anabadilisha uongozi uliopo
analeta wengine matokeo yake bandari yetu haiongozwi kwa ufanisi
unaohitajika,” amesema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema matokeo
yaliyotolewa na BoT yanaonyesha kuwa uchumi hivi sasa unakwenda kwa watu
wachache na kuondoka kwa watu wengi ambao ndio wapo kwenye sekta ya
kilimo, hivyo si jambo la kulifurahia.
“Taarifa hii
inaashiria kwamba watakao nufaika na uchumi ni watu wachache, wamiliki
wa migodi, kampuni za kigeni zinazohusika na utalii na wafanyabiashara
wachache hasa kwenye sekta ya usafirishaji na hivi sasa asilimia 99 ya
mizigo yote inasafirishwa kwa malori,” amesema Zitto.
Akizungumzia
kuhusu kilimo, Zitto amesema: “Kati ya miaka mitatu iliyopita mchango
wa pamba umeshuka kutoka dola 154milioni kwa mwaka mpaka dola 57milioni
kwa mwaka, mikoa sita inayolima pamba ina zaidi ya asilimia 30 ya
wananchi wa Tanzania,” amesema Zitto.
No comments:
Post a Comment