Wednesday 30 March 2016

IJUE HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI, TANZANIA

Ukweli kuhusu  Hifadhi ya Taifa  ya Serengeti
Hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti  Kijiografia  inapatikana  katika  Mkoa wa Mara.  Kihistoria  toka  hapo zamani  katika  hifadhi hii ya Serengeti jamii ya Kabila la Wamaasai ambao  ni jamii ya nilotiki  ambayo  kihistoria  asilia  yake  ni  Kusini  mwa  Sudani  iliishi  kwa miaka  mingi  pamoja na Wanyamapori  katika  hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti.


Ikumbukwe  na ieleweke  ya kwamba  kipindi  cha wakati  huo eneo  hili la Serengeti  ilikuwa  ikihusisha eneo  linalofahamika leo  hii  kama Mamlaka  ya hifadhi ya Ngorongoro ikijulikana  kwa pamoja  kama “Great  Serengeti” kabla ya  eneo  la mamlaka ya hifadhi  ya Ngorongoro  kutenganishwa  mnamo  mwaka  wa 1959 na  kupelekea  jamii  yote ya  kabila la Wamaasai waliokuwa  wakiishi  eneo la Serengeti  kuhamishiwa  katika  Mamlaka ya hifadhi  ya Ngorongoro.
Asili ya jina Serengeti limetokana na lugha ya Kabila la Wamaasai lenye  kumaanisha  uwanda  mpana. 
Nyumbu wahamao katika hifdhi ya taifa ya Serengeti ni moja ya maajabu 7 ya Dunia
MAANDALIZI YA USAFIRI; 
Anza na utafiti  makini unaohusiana  na wadau  wa sekta  ya  utalii  wanaohudumia  shughuli za  utalii katika  hifadhi  hii ya  Taifa  ya Serengeti. Gharama zake zikoje  na zinatofatianaje vipi?  Fedha zinazohitajika na upatikanaji wake.  Mwisho  kabisa  ni mpango  mkakati  wa fedha  na bajeti  ya  matumizi  yenyewe  ya fedha hizo  katika  safari ya matembezi  hifadhini.
KUANZISHWA  KWAKE:
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilianzishwa mnamo mwaka wa 1951. Ikumbukwe  na ieleweke  ya kwamba  mwaka  huo wa  1951 ilikuwa  ikihusisha  kwa pamoja  na eneo  linalofahamika  leo  hii kama  mamlaka  ya hifadhi  ya Ngorongoro  kabla  ya eneo  la  Ngorongoro  kutenganishwa  na kujitegemea kutoka   Serengeti  hapo  mwaka  wa 1959.
ENEO LAKE:
Mpaka  hivi  sasa  ukubwa wa eneo  la hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti  ina  ukubwa  wa kilomita  za mraba  14,763 ( au  sawa  na maili za mraba  5700).  Hivi sasa,  hifadhi  ya  Taifa  ya Serengeti ndio  hifadhi  ya  pili  kwa  ukubwa  baada ya  hifadhi  ya Taifa  ya Ruaha  kuongezwa ukubwa  wa eneo   lake  na kufikia  kilomita za mraba  20,380. 

UFIKAJI  HIFADHINI:
Hifadhi ya Taifa  ya Serengeti  inafikika  umbali  wa kilomita  335 (maili  208 kwa  njia ya barabara  magharibi  ya mji  wa Arusha. Seronera ndio makao makuu  ya hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti.  Ni umbali   wa mwendo wa saa 5 mpaka  6 kutoka mji  wa Arusha  katika  mwendo  wa kawaida.
Watalii wakishangaa baada ya kutua katika uwanja wa Seronera,Serengeti
MAUMBILE ASILIA YA KIJIOGRAFIA HIFADHINI; 
Mto  Grumeti  maarufu  kwa idadi  kubwa  ya  mamba,  majabali  ya  mawe  yenye  mvuto  wa kupendeza,  Tambarare  zenye   nyasi  nzuri  zenye  kupendeza.
HALI YA HEWA USAWA WA BAHARI HIFADHINI;
Hali  ya hewa  kutoka  usawa  wa Bahari  ndani ya  hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti  inaanzia  mita 950  mpaka  1850.  Seronera ndio makao makuu ya hifadhi ya Taifa ya  Serengeti  ni mita 1530.
VIVUTIO VIKUU VYA UTALII HIFADHINI;
Wanyamapori walao nyama kama vile simba, chui na fisi. Wengineo ni kama vile  duma, mbwa  mwitu,  mbweha na wengineo.
Uhamaji wa Wanyamapori  kwa  msimu  maalumu,  Tambarare  zenye  nyasi  nzuri  zenye  kupendeza. Vile  vile  viumbe  hai  ndege  wa  aina  mbalimbali  kama  vile  mbuni.  Hali kadhalika kuna ndege wahamaji kutoka katika sehemu mbalimbali  duniani katika  msimu  husika. 
WANYAMAPORI WAPATIKANAO HIFADHINI;
Wanyamapori  ni wengi  na wa aina  mbalimbali kama vile  mbwa  mwitu, Tumbili (ngedere),  vicheche,  kuro,  ngiri wanyamapori, paa, Taya, kindi,  palahala, korongo,  tohe,  pimbi Wanyamapori, viboko, swala tomi, Kongoni aina  ya cokei,  nguchiro nyumbu, nyegere, digidigi, pongo, Insha, Pofu,  Mhanga,  Nyani,  Nguruwe mwitu,  Mbweha  masikio, mbogo (nyati), chui, simba,  swala pala,  swala granti,  Twiga,  Tembo (Ndovu)  na  wengineo  wengi.
Pundamilia ni moja wa wanyama wanaoambatana na nyumbu wakati wakihama hama
UOTO WA ASILI HIFADHINI; 
Hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti  inaangukia  katika  maeneo  ya uoto wa asili wa maeneo Makame  wa ukanda  wa Somali – Maasai ambapo  uoto  wa asili  wa mimea  asilia  ya  miti  ya migunga na mbabara au  mturituri umetawala.
        Katika  ukanda wa eneo  hili  milimita  za mvua  kwa mwaka  ni  milimita  300 mpaka  700. Vile vile  kuna  uwanda  mpana  wa uoto  wa nyasi (grassland).  Vile vile  uoto  wa asili  wa msitu  unaostawi  kufuata  mkondo wa  mto (Riverine  vegetation). 
WAKATI WA KUTEMBELEA HIFADHINI
Mwezi wa Desemba mpaka Julai kuweza kuona msafara  wa uhamaji wa Wanyamapori kama vile  nyumbu  na wanyamapori  wengineo. Vile vile   mwezi wa Juni  mpaka  Oktaba  kuona  wanyamapori walao nyama  kama vile  simba, chui, fisi,  duma na wengineo  wengi.
HUDUMA ZA CHAKULA; 
Mambo  ya kujiuliza  katika  safari  yenu  ya matembezi  hifadhini,  Je  mtabeba  vyakula  vyenu  wenyewe  vya  kujipikia?  Au  hakuna  ulazima  huo  na badala  yake mtapata  huduma  hiyo katika  sehemu ambazo huduma ya chakula inapatikana.
HUDUMA ZA MALAZI AU KULALA; 
Kama  mtalala  ndani ya hifadhi,  Je  mtapiga  kambi na  katika kupiga kambi  ni lazima  mbebe mahema  yenu?  Au kama hamtalala ndani ya hifadhi ni sehemu gani nyinginezo za huduma hiyo ya kimalazi. 
Kempu ya kulala wageni Serengeti
GHARAMA ZA USAFIRI WOTE;
Umakini katika eneo hili ni la muhimu kwa wahusika ambao ndio waandaaji wa safari ya matembezi hifadhini.
Mambo muhimu ya maandalizi ya usafiri, huduma za chakula, malazi au kulala na mengineyo. Haya yote ndio yatakayokamilisha safari ya matembezi hifadhini. Je  safari yenu ya matembezi hifadhini inaendeka  au haiendani? Jibu litapatikana  baada ya utekelezaji wa mambo  muhimu kukamilka.
MAMBO YA KUFANYA;
Dharura na matatizo mbalimbali hujitokeza katika safari ya matembezi  hifadhini.  Ni vema  na busara  kuwa na utamaduni wa kupeana  mafunzo  yanayohusiana na huduma ya  kwanza na namna  vifaa hivyo  vinavyotumika. 
MAMBO YA KUFAHAMU;
Mawasiliano  ni ya muhimu  na ni lazima  yawepo  kati yenu  na hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti  au makao  makuu  ya Shirika  la hifadhi  za Taifa, Mjini   ARUSHA. Je,  kipindi  ambacho  mtatembelea  hifadhi  hii ni  kipindi  cha wageni  wengi  au  wageni  wachache?  Je mnaweza kupata sehemu ya kupiga kambi au  kulala hosteli? Hili ni suala muhimu la kujiandaa na kujipanga. 
MAMBO YA KUCHUKUA; 
Vifaa vyote muhimu katika safari yenu ya matembezi hifadhini.
HUDUMA ZA MAHITAJI MENGINEYO;
Mambo ya ziada ya mahitaji yanayojitokeza na
upatikanaji wake katika  sehemu  husika. 
MAWASILIANO  MENGINEYO:
Mkurugenzi  Mkuu,
Hifadhi za Taifa, Tanzania
S.L.P. 3134, Arusha, Tanzania.
Simu; 255 – 272503471/2501930-31
Nukushi; 255 272508216
Barua pepe; dg@tanzania parks.com.
info@tanzania parks.com.
Tovuti: www.tanzaniaparks.com
Simu ya Mkononi; 0689-062 369 (airtel)
0767 – 536 140 (vodacom)
Simu ya Mkononi;
0689 – 062 369 (Airtel)
0767 – 536 140 (Vodacom).  
MAWASILIANO HIFADHINI SERENGETI (MOJA KWA MOJA)
0689  - 062 243 (Airtel)
0767 – 536 125 (Vodacom)
MAMBO YA KUZINGATIA HIFADHINI,
Kanuni na taratibu za hifadhi.

No comments:

Post a Comment