Dodoma. Baadhi ya wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini
wametaka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaodai nyongeza ya posho,
wajiorodheshe ili waweze kufahamika kwa majina na wanakotoka.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati
tofauti mjini Dodoma, wananchi hao kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Dar es
Salaam, Arusha na Dodoma, wameipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa
kutowaongezea posho hizo.
Msimamo huo wa Serikali wa kutowaongezea posho
wajumbe hao kutoka Sh300,000 hadi kufikia Sh420,000 au Sh500,000 kwa
siku, ulitangazwa juzi na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Nchemba alisema maombi hayo ya baadhi ya wajumbe,
yamewasilishwa wakati mbaya ambapo Serikali inakabiliwa na mahitaji
muhimu ikiwamo madai ya walimu, wazabuni na ununuzi wa chakula kwa ajili
ya wananchi wanaokabiliwa na njaa.
Naibu Waziri huyo alisema Katiba hiyo
inatengenezwa na Watanzania ambao walipaswa kuwa wazalendo na kwamba
kama wangekuwa ni wataalamu wa kukodiwa, madai yao yangeeleweka.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tecno Group katika Kanda
ya Afrika Mashariki, Chris Martin alisema baadhi ya wajumbe wameonyesha
udhaifu mkubwa kwa kutanguliza maslahi binafsi badala ya umma.
“Binafsi nampongeza sana Mwigulu aliyezungumza kwa
niaba ya Serikali kwani hatuwezi kukubali kila jambo linaloombwa na
waheshimiwa wabunge lazima tupime uzalendo wao,” alisema Martin.
Martin alisema anaamini sio wajumbe wote wanaodai
nyongeza ya posho lakini anataka wanaodai posho waorodheshe majina yao
ili wafahamike.
Martin alisema baada ya kuwafahamu, watamuomba
Rais Jakaya Kikwete, atengue uteuzi wao na kama ni wabunge, basi wajue
watakumbana na adhabu yao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mwanaharakati Kayumbo Kabutali wa mjini Dodoma,
alisema uongozi wa Bunge ulikosea kwa kutoweka wazi bajeti ya posho yao,
ili wajue watalipwa nini na wao wajue watazitumiaje.
“Serikali ilipaswa iwaambie mapema kwamba
tutawalipa kiasi hiki cha posho kwa siku halafu ikapendekeza maeneo ya
bei nafuu ya kulalala na kuishi,”alisema mwanaharakati huyo.
Mtaalamu wa Tiba Asilia, Danny Njau kutoka jijini
Dar, aliwataka wajumbe wanaoona kuwa posho haitoshi, waondoke haraka
bungeni kwa sababu kuna Watanzania walioko tayari kuifanya kazi hiyo kwa
kujitolea.
CHANZO CHA HABARI; Gazeti la MWANANCHI TANZANIA
CHANZO CHA HABARI; Gazeti la MWANANCHI TANZANIA
No comments:
Post a Comment