Rais
Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi (kulia) akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kuhamasisha ulinzi wa Tembo na
Faru pamoja na kupiga vita ujangili kilichoandikwa na Kamati ya Amani ya
Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam jana katika ukumbi wa Kimataifa
wa Mikutano wa Mwl. J.K. Nyerere, Dar es Salaam.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akionesha kitabu hicho kwa
wajumbe walioshiriki hafla hiyo kama ishara ya kukizindua rasmi kwa
niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli.
Rais
Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi (kulia) akiteta jambo
na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi
Mwanasiasa Mkongwe nchini ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama cha
CUF, Prof. Ibrahim Lipumba nakala ya kitabu hicho. Wapili kulia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum.
Picha ya pamoja.
------------------------------------------------------------------
Rais Mstaafu wa Awamu ya pili wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Ally Hassan Mwinyi ametoa wito kwa watanzania
kuongeza juhudi katika kusaidiana na Serikali kupiga vita ujangili hapa nchini.
Wito huo umetolewa jana jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa
kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kilichoandaliwa na Kamati
ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es salaam na kuzinduliwa na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa niaba ya Mhe. Rais,
Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais mstaafu huyo, amesema kumekuwa na tatizo la mauaji ya wanyamapori hapa
nchini ambayo ni dhambi na ni kinyume na kusudio la Mungu kwa kuwa wanyama hao
wana haki ya kuishi kama viumbe wengine.
“Kumekuwa na matukio mengi ya uuaji wa wanyamapori ikiwemo tembo na
faru na hivyo kupunguza rasilimali ya taifa kwa vizazi vijavyo na pia kitendo
hicho ni kinyume na kusudio la Mungu hivyo ni vizuri kuwatunza, kuwapenda,
kuwaendeleza na kuwalinda wanyama hao kwani ni moja ya vivutio vinavyochangia
pato la Taifa” aliongeza Rais Mstaafu Mwinyi.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe
amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mbuga nzuri na bora duniani baada
ya nchi ya Brazil na kusisitiza ni muhimu kwa watanzania wote kutunza
rasilimali za taifa ikiwemo mbuga za wanyama na wanyamapori.
Aliongeza kuwa wanyamapori ni muhimu sana katika maisha ya
kila mtanzania kwa kuwa kupitia utalii wanachangia asilimia 17.5 ya pato la
taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje (foreign currency) hivyo
hakuna budi kwa kila mtanzania kupiga vita ujangili ambao.
Alisema kuwa jumuiya ya ujangili ni kubwa
ambayo inahusisha makundi mbalimbali ikiwemo watengenezaji wa silaha za
kuua tembo, waagizaji wa meno ya tembo, wasambazaji na watu mashuhuri ambao
wanatumia nyumba zao kuhifadhina kununua meno ya tembo.
Kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kimetayarishwa na
kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es salaam kikiwa na lengo la kuwaelimisha
waanadamu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na viumbe vilivyopo kwa faida yao
na vizazi vijavyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa
kamati hiyo ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum
alisema jumla ya vitabu 5,000 vimechapishwa kwa ufadhili wa shirika la
kimataifa la WILDAID, Jumla ya nakala milioni 20 zinahitajika kuchapishwa
katika lugha tofauti na kusambaza katika nchi mbalimbali duniani na hivyo
kuwaomba wadau mbalimbali kuchangia gharama za uchapishaji huo ambao kwa kila
kitabu kimoja kinagharimu dola kimarekani 12.
Akizungumzia uchangiaji huo, Waziri Maghembe
alisema kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TWPF) utachangia milioni
20 kuwezesha uchapishaji wa vitabu hivyo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza
kuunga mkono juhudi za vingozi wa dini na Serikali katika kulinda na kuhifadhi
Malisili za taifa kwa kuchangia uchapishaji wa kitabu hicho na kulinda Malisili
za taifa.
No comments:
Post a Comment