Monday 16 February 2015

MGIMWA : VITA VYA DHIDI YA UJANGILI NI YETU SOTE

Naibu Waziri waWizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Mahmoud Mgimwa amesema kuwa vita dhidi ya ujangili ni vya jamii nzima, wadau na asasi zisizo za kiserikali zisikae pembeni zikidhani Serikali pekee ndio yenye jukumu la kuhakikisha Wanyamapori wanalindwa na kuendelezwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho
Alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa anazindua kampeni ya ‘’Jitokeze tuongee tetea haki za wanyamapori wa Tanzania’’ iliyoambatana na Matembezi ya kupinga ujangili wa wanyamapori ’’ yaliyoandaliwa na na taasisi ya Rafiki Wildlife Foundation.
Matembezi hayo yalianzia Mpingo house na yaliishi katika viwanja vya Mnazi mmoja yakiwahusisha Wananchi, wanafunzi na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alisema kuwa endapo jamii itapewa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kulinda Wanyamapori kila mtu atakuwa balozi wa wenzake kwa kupinga ujangili na kutoa ushirikiano kubaini mtandao wa majangili.
‘’Tunatoa wito kwa jamii ishiriki katika vita hii kwani wanyamapori si wa Wizara pekee bali ni wetu sote’’ Mhe. Mgimwa alisisitiza.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Rafiki Foundation, Mwinjilisti Clement Matwiga alisema jamii inahitaji elimu zaidi hivyo wanahitaji ushirikiano kwa jamii nzima ili waweze kuwa Mabalozi wazuri kwa nchi nzima.
Aidha , Alisema asasi zisizo za kiraia pamoja na wadau wa wanyamapori kusaidiana katika kutokomeza vita dhidi ya ujangili.
Aliongeza kuwa zinahitajika milioni 200 ili kufanikisha kutoa elimu nchi nzima juu ya umuhimu wa kutunza na kuendeleza wanyamapori ambao ni fahari ya taifa ili kutoa mwamko kwa wananchi kupitia kampeni hiyo.

No comments:

Post a Comment