Tuesday, 16 August 2016

KATIBU MKUU MALIASILI, MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI ATOA WITO KWA WADAU WA UHIFADHI NCHINI KUKEMEA VITENDO VYA UINGIZWAJI WA MIFUGO KWENYE MAENEO YA HIFADHI NCHINI


Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ametoa wito kwa wadau wa uhifadhi nchini kukemea kwa nguvu zote tabia ya uingizaji wa mifugo ndani ya hifadhi za Misitu na Wanyamapori nchini kwakuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi na kunahatarisha ustawi wa hifadhi hizo ambazo ni muhimu kiikolojia na uchumi na wa taifa.

Milanzi ametoa wito huo juzi wakati akifunga mafunzo maalum ya kijeshi katika kituo cha Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Mkoani Katavi kwa Mameneja wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Askari wa TANAPA kwa ajili kubadilisha mfumo wa utendaji katika taasisi hizo kutoka wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu (paramilitary) kuboresha utendaji wao wa kazi.

“Mifugo katika hifadhi zetu sio sahihi ni kinyume kabisa cha sheria za nchi, endeleeni kulikemea hili, tusipige siasa kufurahishana kwakua madhara yake ni mengi ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, muingiliano wa magonjwa baina ya mifugo na wanyamapori na kuharibu ubora wa vivutio vyetu” Alisema Milanzi.

Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 Ibara ya 18 (2) inakataza kabisa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, Sheria hiyo inasema “Si ruhusa mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo ndani ya Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Ardhioevu”.

Milanzi alisema kuwa hifadhi za taifa nchini zina umuhifu mkubwa kwa uchumi wa taifa kwakuwa kupitia utalii zinachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje (foreign currency). Aidha sekta hiyo inatoa ajira zaidi ya milioni moja na nusu kupitia huduma za kitalii nchini. 

Mbali na faida za kiuchumi hifadhi hizo pia zina faida nyingi za kiikolojia ambazo ni uhifadhi wa vyanzo vya maji, kusaidia upatikanaji wa mvua na hewa safi kwa viumbe hai ikiwemo binaadamu. Alisema kuharibu hifadhi hizo kwa kulisha mifugo ndani yake ni jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa ni kuhatarisha pia maisha ya binaadamu ambayo yanategemea hifadhi hizo.

Alieleza kuwa Serikali inaenda kulifanyia kazi tatizo hilo pamoja na migogoro mingine ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia suluhu kwa kushirikisha Wizara zinazohusika ambazo ni Ardhi, Kilimo na Mifugo, Sheria na Katiba, Tamisemi, Maliasili na Utalii na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.

Akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo, Milanzi alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uadilifu, nidhamu, ujasiri, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa muda mfupi na hivyo kuwataka kuyatumia kuongeza ufanisi katika kulinda maliasili zilizopo kwenye maeneo yao.

Aliwataka pia wahitimu hao kutafsiri mafunzo hayo na maendeleo ya sekta ya uhifadhi nchini na kuliongezea taifa mapato kwa kuboresha huduma za utalii, kubuni bidhaa mpya za utalii na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Alan Kijazi aliwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuziba mianya yote ya ujangili na kwamba jamii inategemea kuona kazi hiyo kwa vitendo.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na UNDP kupitia mradi wa “Spanest” yalifanyika kuanzia tarehe 15 Julai hadi tarehe 13 Agosti, 2016 kwa kuwahusisha washiriki 69 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Tanapa. Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu yanatemewa kuhusisha taasisi zote za uhifadhi wa wanyamapori nchini kuelekea kwenye mabadiliko ya muundo wa utendaji kazi kutoka mfumo wa Kiraia  kwenda mfumo wa Jeshi Usu (Paramilitary).

No comments:

Post a Comment