Friday, 7 March 2014

Kauli ya M/kiti kutokana na bunge kuahirishwa baada ya malumbano ya Ole Sendeka na Waziri Hamis

Kwenye  bunge maalum la katiba Alhamisi ya March 6 2014 Dodoma, mwenyekiti wa Muda wa Bunge Pandu Ameir Kificho alilazimika kuahirisha semina ya bunge maalum kutokana na kutokea vurugu zilizosababishwa na baadhi ya wajumbe, kupinga kitendo cha kiti cha mwenyekiti kupendelea baadhi ya wabunge.
Vurugu hizo zilianzia pale waziri wa sheria wa Zanzibar ambae pia ni mjumbe wa kamati ya kanuni ABOUBAKAR HAMIS BAKARI alipolalamikia kitendo cha baadhi ya wajumbe kuwasilisha mabadiliko ya kanuni, licha ya majina yao kutopitishwa kwenye kamati ya kanuni ili mapendekezo yao yajadiliwe.

Baada ya hayo, Mbunge wa Simanjiro CHRISTOPHER OLE SENDEKA, ambae ni mmoja wa wajumbe wanaodaiwa kupendelewa alibainisha kwa kuwasilisha mapendekezo yake kwa wakati kwa kusema >>>
‘Na mimi sio dhaifu kwa kanuni na taratibu zinazoongoza mabunge, kazi yetu sio kupeleka marekebisho yetu kwa Aboubakar, kama Aboubakar ana chama chake hoja zangu zinamuuma asimame na kudeclare interest’
Kauli hiyo ilimfanya Aboubakar kuwasha kipaza sauti na kusema >>> ‘Kuanzia mwaka 1980 niko kwenye haya Mabunge, ni miaka 34…… sifikirii kama mtu katoka Simanjiro miaka kumi iliyopita akaja hapa akasema anajua kanuni, sitaki kuombwa radhi lakini ajue kwamba kuna watu wanaojua zaidi kuliko yeye’
Malumbano haya ndio yalifanya Mwenyekiti kuchukua hatua muda huohuo kwa kuliahirisha bunge mpaka jioni ambapo liliendelea na shughuli zake kama kawaida japo baada tu ya kurejea, Mwenyekiti alisema >>> ‘Wale ambao tuliwapa kazi ya kuonana na Waheshimiwa Bakari na Ole Sendeka wameniletea taarifa nzuri kwamba kimsingi wawili hawa wamekubaliana na jambo lile limekwisha, nawashukuru sana hawa Waheshimiwa wangu kwa kulimaliza kwa mioyo kunjufu sana na kupata taarifa kwamba kila mmoja wao hana kinyongo chochote dhidi ya mwenziwe’
Nae James Mbatia alisema >>> ‘tumezungumza na tunamshukuru sana ndugu yetu Waziri wa sheria wa Zanzibar Aboubakar Hamis na kaka yangu Christopher Ole Sendeka kuweza kuridhiana na kuona ni changamoto tu imetokea na sasa kuwa wamoja, sisi sote ni watu wazima na tuko hapa kwa niaba ya Watanzania na kila mmoja wetu anabeba roho za Watanzania elfu sabini na mia nne’

No comments:

Post a Comment