Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh.
milioni moja klabu ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo
vitendo vinavyoashiria ushirikina uwanjani.
Simba ilifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City
ambapo imepigwa faini ya sh. 500,000. Pia imepigwa faini nyingine ya sh.
500,000 kwa makocha wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kuingia
uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo.
Naye mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh.
500,000 kwa kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha
ishara ya matusi kwa kidole.
Mbeya
City imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani
kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za
Yanga na Coastal Union zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa
washabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani wakati timu hizo
zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000
kwa kumpiga mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa
Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtukana refa kwenye mechi
dhidi ya Mbeya City.
Pia mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh.
500,000 kwa kosa la kupigana uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti
United ambapo vilevile atakosa mechi tatu za ligi. Coastal Union
imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kumrushia chupa za maji
kipa wa Mbeya City.
Nayo JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika
uwanjani kwenye mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Vilevile wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa
barua ya kufanya marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa vile havina
hewa ya kutosha.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini
kutokana na makosa mbalimbali ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli
(sh. 200,000), Majimaji (sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na
Transit Camp (sh. 200,000).
Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro, John Tamba atapelekwa kwenye
Kamati ya Maadili kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili katika mechi
dhidi ya Burkina Faso.
Kiongozi wa Lipuli, Hamis Kiemba na wachezaji Boniface Sawaka, George
Enock na Green Paul watapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kutokana na
utovu wa nidhamu waliofanya kwenye mechi dhidi ya Kimondo.
Naye mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT Kanembwa aliyelalamikiwa
uhalali wake na Polisi Tabora suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.
No comments:
Post a Comment