Monday, 27 June 2016

TAARIFA KWA UMMA JUU YA USHIRIKI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KATIKA MAONESHO YA 40 YA BIASHARA YA KIMATAIFA - SABASABA

Wizara ya Maliasili na Utalii itashiriki katika Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 8 Julai, 2016 katika viwanja vya Mwalimu Julius. K. Nyerere, Dar es Salaam.
Wizara itakuwa na washiriki kumi na sita (16) ambao ni Idara pamoja na Taasisi zake mbalimbali. Idara zitakazoshiriki ni Utalii, Wanyamapori, Mambo ya Kale na Misitu na Nyuki.
Kwa upande wa Taasisi ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii, Makumbusho ya Taifa, Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na Vyuo vya Wanyamapori (Mweka, Pasiansi na Likuyu Semaganga).
Taasisi nyingine ni Vyuo vya Misitu na Nyuki (Olmotonyi, FITI Moshi na Chuo cha Nyuki Tabora), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wakala wa Mbegu za Miti, Taasisi ya Utafiti wa Misitu na Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Washiriki wote hao watakuwa kwenye banda moja la MALIASILI, Wizara inawakaribisha wananchi wote kwenye banda hilo waweze kujionea na kuelimika na mambo mbalimbali yanayohusu Utalii, Ufugaji wa Nyuki, Uhifadhi wa Misitu, Malikale na Wanyamapori.
Aidha, Wizara itatoa punguzo kwa watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa gharama nafuu. Safari ya kwenda na kurudi kwa watoto itakua Tsh. 10,000 na watu wazima Tsh. 20,000. Safari ya kulala itakuwa Tsh. 50,000.
Pia katika maonesho hayo itakuwepo fursa ya kuwaona wanyamapori hai mbalimbali kama vile Chui, Nyoka, Ndege wa aina mbalimbali pamoja na SIMBA.
Kaulimbiu ya Maonesho hayo mwaka huu inasema “Tunaunganisha Uzalishaji wa Masoko”
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii
27 Juni, 2016.

No comments:

Post a Comment