Wednesday 26 February 2014

KUTOKA BUNGE LA KATIBA; Serikali tatu zawatesa wajumbe

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiweka msimamo wa kupinga muundo wa serikali tatu, baadhi ya wajumbe wameelezwa kusikitishwa na mjadala kujikita kwenye muundo wa serikali.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, walisema mazungumzo makubwa yaliyotawala ni muundo wa serikali badala ya kufikiria kujadili mambo muhimu yenye masilahi ya taifa.
 Mmoja wa wajumbe hao, Dk. Pudenciana Kikwembe alisema ni vema kwa sasa wajumbe wakawaza mambo yenye masilahi kwa taifa badala ya kufikiria zaidi ya masuala ya Muungano.
  “Hapa napata mashaka sana kama kweli katiba hii itakuwa na maana kwa Watanzania walio wengi kama kweli tutaendelea na msimamo ambao unaonekana kujengeka kwa wajumbe wengi ambao wapo katika bunge hili. 
“Kila mtu akili yake inawaza zaidi juu ya muundo wa serikali, lakini sijasikia kama kuna watu ambao wanajikita zaidi katika masuala ya msingi na kuonyesha nia ya wajumbe kuweka vipaumbele ambavyo vitawafanya Watanzania kunufaika kutokana na rasilimali zao.
 Job Ndugai, alisema Bunge hilo hivi sasa linaonekana litatawaliwa na mijadala mikali kuhusu muundo huo na mamlaka ya rais kwa kuwa mambo hayo yamepewa msukumo mkubwa na wanasiasa na vyombo vya habari.
Alisema tayari mambo yameshaanza kuonekana yatakuwa magumu katika hatua za awali ambapo wabunge wengi walikuwa wakijadili bila utaratibu huku wengine wakionekana kubeba misimamo yao.
  “Si vibaya kuwa na msimamo lakini cha msingi hapa tunatunga Katiba ya taifa, hivyo ni lazima tubishane kwa hoja na kushawishiana kwa lengo la kutengeneza Katiba Mpya nzuri zaidi,” alisema.

No comments:

Post a Comment